SHIRIKA LA NYUMBA ZANZIBAR
________________________________________________________
TAARIFA KWA UMMA
UHARIBIFU WA TASWIRA NA UIMARA WA NYUMBA ZA MAENDELEO
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia awamu mbali mbali za Uongozi ilijenga nyumba za maendeleo zikiwemo za Michenzani, Kilimani, Kikwajuni, Gamba, Mpapa, Makunduchi na Mombasa kwa Mchina kwa upande wa Unguja. Aidha kwa upande wa Pemba nyumba hizo zimejengwa maeneo ya Machomane na Madungu Chakechake, Mtemani wete, Micheweni na Mkoani. Lengo la ujenzi wa nyumba hizo ni kuwapatia wananchi makaazi bora na salama. Vile vile katika awamu ya nane (8) chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi inaendelea na azma ile ile ya kuboresha na kuwapatia wananchi wake makaazi bora na salama kwa kujenga nyumba za makaazi sehemu mbali mbali.
Katika miaka ya hivi karibuni kumejitokeza tabia ya wakaazi wa nyumba za maendeleo iwe wapangaji wa Shirika la Nyumba au wamiliki binafsi kuharibu taswira za nyumba hizo kwa kufanya matengenezo yasiyofuata sheria na taratibu za Shirika, kubadilisha muundo wa zamani wa nyumba, Matengenezo yanayohusisha kuvunja muhimili wa nyumba “structure”, kuchimba kuta, kuvunja kuta, kukata bimu, kuvunja sakafu za nyumba hizo na kutengeneza muhimili wa nyumba “structure” mpya, kuvunja muhimili wa nyumba na kuweka maduka, saluni, Mkahawa, kuweka vipaa vya zege na kuweka uwa wa makuti au “mapolo”. Matengenezo hayo husababisha ubovu au uharibifu wa nyumba hizo na kuharibu muonekano wa asili wa majengo hayo au kuleta ubovu wa nyumba hizo.
Kila mtu ajue kuwa nyumba hizi ni za ghorofa yanayotumiwa na watu wengi hivyo ukiharibu nyumba moja inaleta athari kwa jengo zima ambapo unaweza kuathiri watu wengi.
Kwa mujibu wa Sheria ya Shirika la nyumba Zanzibar Sheria namba 6/2014 kifungu namba 7(2b) na pia kupitia kanuni ya 6 na 23 ya Kanuni Namba 109/2015 ya Sheria ya Kondominio Namba 10/2010 ambapo zinaelekeza kuwa matengenezo yeyote ya Nyumba za maendeleo lazima yaombwe kwa maandishi kupitia Shirika la Nyumba na kujibiwa kwa maandishi baada ya wataalamu wa Shirika kujiridhisha. Tunapenda kuwakumbusha wakaazi wote wa nyumba za maendeleo kuwa matengenezo yeyote yanayoharibu taswira ya ujenzi wa asili wa nyumba hizo HAYARUHUSUWI iwe kwa mpangaji wa Shirika au mmiliki binafsi na kufanya hivyo ni uvunjaji wa taratibu za makaazi wa nyumba hizo. Aidha kwa upande wa uwekaji wa madirisha inatakiwa kuweka ndani ‘grill’ katika madirisha kama inavyoonekana Bloki No.1 Michenzani, Madungu Chakechake na Mtemani Wete kwa nyumba ambazo zilizotengenezwa na Shirika. Pia kuweka ‘tiles’ za gundi katika ‘floor’ badala ya kutumia saruji.
Hivyo basi Shirika la Nyumba Zanzibar linawaatarifu wakaazi wa nyumba za Maendeleo na umma kwa ujumla kutokubadilisha muundo wa zamani wa Nyumba za Maendeleo. Shirika linawataka wale wote waliofanya uharibifu wa nyumba hizo kurekebisha kwa kurejesha muonekano na muundo wa awali, kuacha mara moja kuendelea na ujenzi au matengenezo yoyote ambayo hayajafuata taratibu na sheria za Shirika pia yanalenga kuharibu taswira ya ujenzi wa awali.
Taarifa hii imetolewa na:
MKURUGENZI MKUU
SHIRIKA LA NYUMBA
ZANZIBAR