Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar, Bi Mwanaisha Alli Said ameendeleza ziara yake kisiwani Pemba na kupata nafasi ya kukutana na Afisa Mdhamin wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini Muhandisi. Suleiman Hamad Omar ambae kabla ya nafasi yake hio, alikua Mkurugenzi wa Ofisi ya Shirika la Nyumba Pemba. Pamoja, walibadilishana mawazo na kujadili mambo mbali mbali ya maendeleo yanayohusiana na Shirika la Nyumba kwa upande wa Pemba.
Vilevile, Bi. Mwanaisha alifanya ziara ya ukaguzi wa nyumba za Maendeleo za Micheweni na Nyumba za Vijiji za Maziwang'ombe kwa kufanya mazungumzo na wapangaji aliowakuta na kuwashajihisha kulipa kodi kwa wakati ili Shirika liweze kuzifanyia matengenezo nyumba hizo pamoja na kuzitunza ili ziweze kuwafaa zaidi.
Wakati huo huo, Mkurugenzi alifanya ziara kwenye nyumba za Maendeleo zilizopo Wete na kukutana na Sheha wa Shehia ya Mtemani Bw. Mrisho Juma Mtwana na kufanya nae mazungumzo kuhusu nyumba hizo na kuomba mashirikiano yake kwenye masuala yote yanayohusu nyumba za Shirika zilizopo kwenye Shehia yake.
Pia alikutana na wafanyakazi wa Ofisi ya Shirika la Nyumba ya Wete na kufanya nao kikao cha kujadili mambo mbali mbali juu ya majukumu yao na kuskiliza changamoto zinazowakabili. Mkurugenzi aliwasihi wafanyakazi hao kushirikiana vizuri na wafanyakazi wenzao wa Chakechake ili wazidi kuleta maendeleo kwenye Shirika. Aliwataka waje na mikakati mipya ya kukusanya kodi na kuongeza pato ili Shirika liweze kufanya kazi zake kwa vizuri na kufanikisha malengo yake.