
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar, Bi. Mwanaisha Alli Said, alifanya ziara ya ukaguzi wa maeneo ya uwekezaji ya Shirika yaliyopo Chakechake pamoja na Maduka ya biashara na kufanya mazungumzo na baadhi ya Wapangaji wa maduka hayo ambapo aliwashajihisha kulipa kodi kwa wakati na kufuata masharti ya mikataba yao kwani kutokufanya hivyo kutapelekea Shirika kuchukua hatua za Kisheria juu yao.
Aidha, alitembelea kwenye Nyumba za Vijiji za Kengeja na Mwambe pamoja na Nyumba za Maendeleo za Mapinduzi zilizopo Mkoani ambapo alipata nafasi ya kuongea na Diwani Mhe. Mrisho Juma Mtwana na kumuomba ushirikiano wake kwenye masuala yote yanayohusiana na Nyumba za Shirika zilizopo katika Wadi yake.
Alimalizia ziara yake kwa kufanya kikao na wapangaji wa nyumba za Madungu na Machomane kwa ajili ya kujitambulisha kwao na kuwashajihisha kulipa kodi kwa wakati ili Shirika liweze kumalizia na matengenezo ya nyumba za Madungu na kuweza kufanya matengenezo kwenye nyumba nyengine zaid pamoja na kujenga nyumba kwa ajili ya kuwapatia Wazanzibari wengine makaazi bora. Na aliwasihi wapangaji hao kufuata Sheria na kuacha tabia za kukodisha au kutoa vilemba nyumba za Shirika na atakaejulikana anafanya hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
